Wednesday, January 11, 2012

LISHE BORA KWA WATOTO HUWAPA MAENDELEO MAZURI SHULENI

LISHE bora kwa watoto ni changamoto kwa wazazi wengi. Hii ni kutokana na umuhimu wake kwa afya ya mtoto kiakili na kimwili.

Utafiti unaonyesha kuwa ni muhimu kujumuisha lishe bora katika mpangilio wa mtoto anayesoma hasa katika kipindi cha mitihani ili kumsaidia kufaulu katika mtihani wake.

Utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa wazazi wengi huwa mbali na watoto wao pale wanapojiandaa na mitihani. Huwa mbali katika kuwaandaa vyema tangu kiakili hadi katika kuwapatia lishe bora.

Vile vile, utafiti huo unaonyesha kuwa jinsi mwili unavyozidi kuwa na afya bora, ndivyo ubongo unavyozidi kupata nguvu na kijana wako anavyoweza kusoma vyema na kuwa na akili nzuri.

Wazazi wengi huzingatia lishe bora kwa watoto pale wanapokuwa wagonjwa na kusahau kuwa lishe bora ni muhimu wakati wote wa ukuaji wa mtoto.

Lakini, vipo vyakula vinavyofaa kwa watoto hususan wale wanaojiandaa na mitihani. Wataalam na washauri katika masuala ya lishe bora kwa watoto wanakumbusha kuwa wakati huu wa mitihani, watoto wanahitaji chakula kitakachoimarisha afya na utendaji kazi wa ubongo wake na kisichomletea usingizi na kitakachomsaidia kufikiri vizuri.

Mfano vyakula vya wanga vinaupa mwili nguvu inayohitajika kufanya kazi. Hakikisha unavigawanya kwa siku nzima kwa kumpa kidogo kidogo katika kila mlo. Vyakula hivi ni kama wali, chapati viazi na muhogo.

Epuka vyakula vyenye sukari nyingi ambavyo vitampa nguvu kwa muda mfupi tu. Aina hii ya vyakula haishibishi ingawa vinampa mtoto nguvu kwa muda mfupi.

Vyakula vya aina hii pia kwa kuwa havina protini vitamin na madini kwa usawa. Aina hii ya vyakula humuacha mtoto akijihisi mzito na mwisho kusinzia.

Chumvi nyingi nayo ni hatari na inaweza kupandisha shinikizo la damu. Chakula chenye mafuta ni hatari kwani kitasababisha usingizi.

Hakikisha chakula cha mwanao, kina aina moja ya chakula kilichojaa protini. Vyakula hivi ni kama samaki, mayai, nyama isiyokuwa na mafuta, maziwa ya mgando, maharage. Aina hii ya vyakula mbali na protini itampa mtoto vitamin na madini.


Kwa upande wa vinywaji ni muhimu sana mtoto kunywa maji ya kutosha. Pia anywe maji ya matunda halisi (juisi).


Ni muhimu kuhakikisha kuwa mtoto anapata vitamin na madini ili kuimarisha afya ya akili na mwili pale anaposoma. Vyakula vyenye madini ni kama nyama ya ngombe, mbuzi na kondoo pamoja na mboga za majani kama spinachi.

Sio vizuri sana kumpa mtoto vidonge vya ziada vya kujaza madini asiyokuwa nayo. Ni vyema ale vyakula halisi kwani vitampa zaidi ya madini anayohitaji. Kumbuka kumpa matunda ya aina mbalimbali kama machungwa, maembe, embe na karoti.

Pia ni vizuri mtoto ale kwa wakati unaofaa. Usipende kumshindisha mtoto na njaa wala usipende ale ovyo ovyo. Chakula kingi huchukua muda kusagwa na kutumia muda mwingi wa ubongo.

Kifungua kinywa wakati wa asubuhi ni muhimu na lazima kwa mtoto hasa katika kipindi cha mitihani. Ni vyema kifungua kinywa kiwe na protini, madini na mboga pamoja na tunda. Kumbuka kupata virutubisho mapema kutasaidia mwili kuvigawanya kwa siku nzima.

Matunda ni moja ya vyakula bora kwa akili. Sukari ya asili katika matunda, hutoa nguvu safi ya kudumu katika mwili kuliko ile sukari inayotengenezwa viwandani.

Mwisho mpe mwanao nafasi ya kupumzika. Apate hewa safi na apumzishe mwili. Pia wakati wa kula asifanye jambo linguine zaidi ya kula ili afurahie chakula chake.

No comments:

Post a Comment